VICOBA WAJITOLEA KUFANYA USAFI KITUO CHA AFYA CHALINZE

Ben Komba/Pwani-Tanzania

WANANCHI wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kujitolea kwa kusaidia sehemu zinazotoa huduma za kijamii badala ya kusubiri serikali au wafadhili.

Hayo yamesemwa na diwani wa kata ya Bwiringu Nasa Karama, alipokuwa akikabidhi msaada wa sabuni, Juisi na matunda kwa wagonjwa kwenye kituo cha afya cha Chalinze uliotolewa na asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya kata ya Lugoba ya Tushikamane Kuinua Wanawake (TUKUWA) VICOBA.

Karama amesema kuwa kujitolea si lazima mtu awe na utajiri au fedha nyingi kama baadhi ya watu wanavyofikiria hivyo kushindwa kusaidia watu au sehemu zinazohitaji msaada.

Karama ameongeza Mmefanya jambo la kiungwana kwani hata watu wenye uwezo na mali wanashindwa kujitolea hata sabuni ambazo hazihitaji uwe na mamilioni ni moyo tu wa kujitolea,

Aidha amefafanua kuwa maeneo yanayotoa huduma au watu wenye mahitaji hawahitaji vitu vikubwa kwani mahitaji ni mengi hata vitu vidogo vinahitajika ambavyo havina gharama kubwa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa asasi hiyo Maria Mbaji amesema kuwa waliamua kusaidia sabuni pamoja na kujitolea kufanya usafi ikiwa ni sehemu ya wao kama jamii kujitolea kwenye sehemu ya kutolea huduma.

Mbaji amesisitiza kuwa mbali ya kujiunga kwa lengo la kujiinua kiuchumi pia wamekuwa wakitoa misaada kwa watu wenye mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwa yatima, wajane na watoto waishio kwenye mazingira magumu.
END. 
 

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA