CHANGAMOTO YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
HUKU zoezi la usajili na utambuzi wa watu Mkoani Pwani ili
kupata vitambulisho vya utaifa likiendelea kumejitokeza changamoto kutokana na
Ofisi za Serikali za Mitaa kuwatoza wananchi shilingi 1,000 kwa ajili ya kupata
barua za uthibitisho wa ukaazi.
Baadhi ya wakazi wa
Mitaa ya Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha wamelalamika kutozwa kiasi hicho
cha fedha jambo ambalo walisema kuwa huenda ikasababisha watu wengi kushindwa
kujiandikisha hali itakayosababisha wakose vitambulisho vya utaifa.
Moja ya wakazi wa mtaa
wa Tangini Juma Shamte alisema kuwa taratibu haziruhusu barua hizo kutozwa
fedha bali zinatolewa bure hivyo kutoza malipo ni kinyume cha utaratibu.
“Baadhi ya watu hawana
vithibitisho vyovyote ambapo taratibu zinawataka endapo hawana uthibitisho wawe
na barua ya utambulisho toka kwenye Mtaa anaoishi,” alisema Shamte.
Aidha alisema kuwa wao
walitangaziwa kuwa zoezi hilo ni bure na hakuna malipo yoyote lakini
wanashangaa kutozwa fedha hizo na kuwapa mzigo michango kupata huduma ambazo
hutolewa bure.
“Fedha hizo ni mzigo
kwani mbali ya kutoa fedha hizo wanatakiwa kulipa shilingi 3,000 kwa ajili ya
kupiga picha za paspoti saizi ambazo wanapiga sehemu mbalimbali si kwenye ofisi
hizo za Mitaa kwa ajili ya kuwekwa kwenye barua hizo za utambulisho,” alisema
Shamte.
Mkazi huyo alisema
kuwa huwabidi kuwa na kiasi cha shilingi 4,000 ambapo 1,000 ya barua ya
uthibitisho toka kwenye Mtaa na 3,000 kwa ajili ya picha ili waweze kujiandikisha
kupata vitambulisho hivyo vya utaifa ambavyo ni muhimu kwa wananchi kwa ajili
ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba mikopo.
Akizungumzia kuhusiana
na changamoto hiyo Diwani wa Kata ya Maili Moja Andrew Lugano alisema kuwa
kutozwa fedha hizo ni kinyume na utaratibu hivyo kwa ile mitaa inayofanya hivyo
inapaswa kuacha na kuwapatia bure barua hizo.
“Kutoza fedha ili
kupata barua hizo ni ukiukwaji wa taratibu na kuwataka viongozi hao wa Mitaa
kuacha kufanya hivyo ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kama Serikali ilivyopanga,”
alisema Lugano.
Hata hivyo badhi ya
wakazi wa mkoa huo wameiomba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA kwa
kushirikiana na Halmashauri kutoa matangazo zaidi juu ya zoezi hilo kwani
baadhi ya watu hwana taarifa hasa wale waliopembezoni mwa Mitaa na Vijiji vya
mkoa huo jambo ambalo litasababisha wengi kutoshiriki zoezi hilo
Mwisho.
Comments
Post a Comment