AUWA MTOTO WA MIAKA 3, AJARIBU KUTOROKA LAKINI AKAMATWA
Ben Komba/Pwani-Tanzania/09-10-2013/13:38
Kibaha tarehe 09 Oktoba, 2013. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Bahati Andulile maarufu kama Ester umri miaka 18 mfanya kazi wa ndani kwa Bw. Alan Mziray kwa kosa la mauaji ya mtoto wa bosi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameeleza kuwa mwili wa marehemu aitwaye Arafat Alan umri miaka 3 na miezi 4 ulikutwa kwenye dimbwi la maji machafu katika eneo la kiwanja cha mpira Maili Moja majira ya saa 07:20 asubuhi Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kamanda Matei ameongeza kuwa mfanyakazi huyo wa ndani kwa Bw. Alan aliondoka na mtoto huyo tangu tarehe 06/10/2013 majira ya saa 4.00 asubuhi baada ya kutumwa kwenda sokoni kununua mahitaji lakini hakurudi tena na mtoto huyo hadi mwili wake ulipokutwa kwenye dimbwi la maji machafu akiwa amekufa.
Mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi na Daktari ulikutwa ukiwa na majeraha Kichwani eneo la utosini na baada ya kumhoji msichana huyo amekiri kuhusika kwa tukio hilo na kudai kuwa alimpiga na kitu kizito utosini mtoto huyo.
Mtuhumiwa huyo ameeleza kuwa sababu za kumuua marehemu ni kutokana na yeye kuwa mgeni wa eneo ambalo alikuwa akifanya kazi na baada ya kupotea njia ya kurudi nyumbani, na kulala porini na mtoto huyo lakini kutokana na mtoto huyo kuwa analia aliona akimkera na kuamua kumpiga kwa kutumia kipande cha gongo kichwani.
Mwili wa mtoto huyo ulibainika na mpita njia na baada ya taarifa kufikishwa katika kituo cha Polisi Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 08/10/2013 katika eneo la stendi Mailimoja akiomba usafiri wa kwenda nyumbani kwao Mbeya.
Comments
Post a Comment