TAGIDO YAWANOA WAKAZI TALAWANDA
Na Omary Said, Bagamoyo
Juni 30
TAASISI ya TAGIDO inayojihusisha na utoaji wa elimu ya ujasiriamali
wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani juzi imeendesha mafunzo ya siku moja
kwa vikundi 58 vyenye wanachama 293 ndani ya Kata ya Talawanda
wilayani hapa.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo katika kijiji cha Magulumatali ofisa
wa TAGIDO Hamza Mfuame alisema kuwa wamekuwa wakiendesha mafunzo
ambayo yamekuwa na faida kwa vikundi na wanachama ambapo tayari
vikundi vimenufaika na mikopo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.
"Asasi yetu ambayo ina makao yake Bagamoyo imejikita zaidi katika
utoaji wa mafunzo kwa vikundi vya ujasiriamali ambapo vikundi
mbalimbali na wanachama wake wamenufaika na elimu hii na hatimaye
kukopa fedha na kujikwamua kwenye shughuli za kimaendeleo," alisema
Mfaume.
Nae Mwakilishi wa NMB Mark Andulu alisema kwamba uongozi wa Makao
Makuu wa benki umeelekeza nguvu zake maeneo ya vijijini kwa lengo la
kuwafikia wakazi wake ambao wanahitaji huduma hiyo na kuwa kuna
akaunti mpya imeanzishwa inayojulikana kwa jina na chapchapo akaunti
ambayo haia masharti katika kuifungua," alisema Andulu.
Kwa upande wake Mutisya John kutoka asasi ya Afrika inayojihusisha na
elimu ya namna ya uanzishaji wa biashara aliwaeleza wajasiriamali hao
kuwa kabla ya kufungua akaunti kitu cha kwanza kutambua aina ya
biashara na soko na ambapo alisema ndio baadhi ya mambo muhimu.
Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo ya siku moja, diwani wa Kata
hiyo Said Zikatimu aliwataka wanavikundi hao kuzingatia mafunzo ili
waweze kujikwamua kwenye shughuli zao za biashara na hatimaye kuelekea
katika mafanikio za kazi zao.
"Nitumie nafasi hii kuwaeleza kwamba serikali ya vijiji hivi
inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi itakuwa bega kwa bega na
wanavikundi wataokopa ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na
hatutarajii wanavikundi hao kufikishwa mahakamani katika mchakato
huo," alisema Zikatimu.
MWISHO.
WADAU WA MAENDELEA WALILIA MRADI WA MAJI
Na Omary Said, Bagamoyo
Juni 30
WADAU wa Maendeleo ya Maji kutoka vijiji vya Kitonga na Kidogozero
Kata ya Vigwaza wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamelalamikia
kusuasua kwa mradi wa maji kwenye vijiji hivyo hali inayochangia
wakazi hao kutumia maji yasiyo safi na salama.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha kujadili
changamoto hiyo, Mwenyekiti wa wadau hao Said Ndaro alisema kuwa mradi
umefikishwa kwenye vijiji hivyo bila serikali za vijiji na wadau hao
kujulishwa hali ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wakazi.
Akijibia hilo Diwani wa Kata ya Vigwaza Mbegu Dilunga alisema kuwa
mradi huo umewashiriisha viongozi wote wa vijiji pamoja na wananchi
kwa maeleza kulifanyika vikao kati ya serikali ngazi ya Kata na wilaya
pamoja na wananchi, lakini amekiri kuwepo kwa dosari wakakti wa
kuendeshwa kwa mradi huo.
Ndaro alisema kwamba mradi huo umeingizwa katika vijiji hivyo bila
kujulishwa viongozi wa serikali, huku mradi wenyewe ukitekelezwa
kinyume cha ushauri wa wananchi ambao walimtaka mkandarasi kampuni ya
Ndaro aboreshe huduma ya maji iliopo lakini waling'oa miundombinu hiyo
na kuweka mipya hali ambayo imesababisha hata maji yaliyokuwa
yanapatikana awali kutokuwepo tena.
"Awali tulikuwa tunapata maji kupitia mradi ambao ulikuwepo kwa miaka
mingi, lakini mkandarasi aliyepewa kazi hii ameng'oa mabomba hayo na
kuweka yake ambayo hayana ubora na cha kushangaza mpaka sasa hatujui
lini mradi utakamilika isitoshe mpaka sasa kuna usumbufu mkubwa wa
maji," alisema Ndaro.
Naye mmoja wa wakazi Rahima Ally aliwaeleza waandishi kwamba wakazi wa
Kitonga wanatumia maji ambayo pia yanatumiwa na ng'ombe na mbaya zaidi
hata mbwa wanaingia katika mai hayo na kusababisha magonjwa ya
mripuko.
"Kama mnavyoyaona haya ndiyo maji tunayotumia sisi wakazi wa Kitonga,
ng'ombe na mbwa wanaingia tunapotaka kuchota kwa ajili ya shughuli
zetu tunalazimika kuwafukuza ndio tunachota na kwenda kuyatumia,"
alisema Rahima.
Kwa upande wake Katibu wa Wadau hao Rashid Mpesa alisema kuwa
wamemwandikia barua Mbunge wao Shukuru Kawambwa iliyoainisha
changamoto mbalimbali kuhusiana na kusuasua kwa mradi huo hivyo
wamemuomba afike kuangalia hali ilivyo.
Akizungumzia hayo diwani Dilunga alisema kuwa kimsingi mradi umefika
na kabla walijulishwa viongozi wa serikali zote za vijiji viwili,
wadau wa maendeleo ya maji sanjali na baadhi ya wananchi kupitia
mikutano iliyoitishwa kwa lengo la kujulishwa kwa mradi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment