HABARI ZA POLISI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Kibaha tarehe 19 Julai, 2013 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Mkoa wa Pwani imemuhukumu Bw. Amosi Mwita Chacha umri miaka 40, Mkazi wa Miembe Saba Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani kwenda jela miaka 6 baada ya kukutwa na hatia katika Kesi ya Wizi wa vocha za tigo pamoja na kesi ya Kukutwa na Mihuri bandia.
Mtuhumiwa huyo amekutwa na hatia kwa makosa yote mawili yaliyokuwa yakimkabili Katika kesi iliyokuwa ikisikilizawa na Hakimu Mkazi, Mhe. Aziza Mbadyo.
Mwendesha mashitaka wa Serikali Bw. Emmanuel Maleko  ameeleza mbele ya  mahakama kuwa mtuhumiwa mnamo tarehe 03 Juni 2013 huko eneo la Sinza Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam alikutwa akiwa na Mihuri ya Afisa Mtendaji Mtaa wa kwesimu pamoja na wa Kituo cha Ukaguzi wa Maliasili cha Soni kilichopo Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mihuri hiyo katika usafirishaji wa mali asili kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam kwa lengo la kuweza kuvuka vizuizi vya mali asili vilivyopo kwenye barabara kuu.
Aidha,Bw. Maleko ameieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Kibaha Mkoa wa Pwani akiwa na vocha za muda wa hewani za kampuni ya simu ya tigo zenye thamani ya Tsh. 5,000,000/= akizisafirisha kwenda Tanga akitokea Dar es Salaam.
Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali ameongeza kuwa makosa yote hayo mawili aliyokutwa na hatiya dhidi yake,  Bw. Chacha anadaiwa kuyatenda kwa nyakati tofauti.
Akisoma hukumu hiyo kwa muda wa saa moja na nusu, Mhe. Mbadyo alisema kuwa Mahakama imeridhika na maelezo ya upande wa Jamhuri hivyo imemtia hatiani Amosi Mwita Chacha kwenda Jela miaka sita (6) ambapo katika kosa la Wizi wa vocha za tigo alihukumiwa miaka minne (4) na kosa la Kukutwa na Mihuri bandia alihukumiwa miaka miwili (2) hivyo adhabu zote mbili zitakwenda pamoja na atatakiwa kwenda Jela miaka sita alisema Bi. Mbadyo.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kibaha tarehe 19 Julai, 2013. Mkazi wa kijiji cha Nyanduturu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Ally Said Makakatau umri miaka 46 amepoteza maisha baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kukatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 00:30 usiku baada ya watu wapatao sita kuvamia nyumbani kwa Bw. Makakatua na kuvunja mlango wa nyumba aliyokuwemo kisha kumshambulia kwa kutumia mapanga kichwani, mkononi na miguuni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Juma Yusufu Ali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameeleza kuwa watu hao walivamia katika nyumba hiyo na kumtaka marehemu kuwapatia pesa ambazo alikuwa amepata za mauzo ya mafuta aliyokuwa amefanya jioni ya siku hiyo na baada ya kukataa kutoa ndipo waliamua kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Kamishina Juma ameongeza kuwa watu hao mbali ya kuvunja  nyumba ya mfanyabiashara huyo, pia walivunja duka na kuchukua pesa taslimu Tsh. 2,800,000/= ambazo zilikuwa ni za mauzo ya mafuta.   
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawasaka watu hao na kuwataka wanachi kuwapatia taarifa zitakazo saidia kuweza kuwapata waliohusika na tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa Daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefanikiwa kumkamata Bi.Tatu Abdallah umri miaka 37 Mkazi wa Ikwiriri Wilaya ya Rufiji kwa kosa la kumuua Azani Rashidi Mehekwa umri miaka 35 baada ya kumtuhumu kutembea na mzazi mwenzake Omari Abdallah.
Bi. Tatu anadaiwa kutenda kosa hilo usiku wa tarehe 17/07/2013 kisha kukimbia lakini baada ya msako uliondeshwa kwa kushirikiana na raia wema hatimaye aliweza kukamatwa hapo jana.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Juma Yusufu Ali amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa ni mke wa Bw. Omari Abdallah kabla ya kutalakiana na ameeleza kuwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili dhidi yake.
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu ishirini (20) raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchi bila kibali.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 01:30 usiku eneo la Mkuranga Mjini Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Juma Yusufu Ali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameeleza kuwa watu hao walikamatwa na askari waliokuwa doria wakiwa wanatembea makundi makundi  katika eneo la Mkuranga Mjini.
Kamishina Juma ameeleza kuwa watu hao baada ya kuwa hoji walibaini kuwa walishushwa kwa gari na kuamua kutembea ili kuweza kuvuka kwenye eneo lililokuwa na kizuizi cha Polisi.
Raia hao wa Ethiopia waliokamatwa ni Habtamu Ambesi umri miaka 21, Yesak Mishamo umri miaka 19, Biuk Moltumo umri miaka 20, Apepe Eshetu, umri miaka 20, Mesfin Taddes, umri miaka 20, Debero Shenke, umri miaka 20, Teamat Kesse, umri miaka 18, Gerenu Debere, umri miaka 20, Tofek Anshabo, umri miaka 25, Lomabebo Gahtchowo, umri miaka 20, Asle Mugoro, umri miaka 20, Chakiso Eriso, umri miaka 20, Wondimu Birhanu, umri miaka 18, Mulatu Menuru, umri miaka 22, Gezahegn Lire, umri miaka 21, Tileahnu Desta umri miaka 20, Muly Geta umri miaka 21, Abdi Mohamed umri miaka 22, Ali Lonsako umri miaka 25, Johann Bincebo umri miaka 20, Degnat Tesema umri miaka 16, Femasene Fitamo umri miaka 17 pamoja na Temaggne Kebeda umri miaka 25.
Aidha Kamanda Juma amesema pia Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata John Kishaki Kataraya umri miaka 50 mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam ambaye alikuwa akiwasafirisha wasomali hao.
Kamanda Juma amesema kuwa watu hao waliingia nchi kwa kutumia njia ya usafiri wa gari kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kusini ili kuweza kwenda nchi jirani ya Msumbiji.
Ameongeza kuwa watakabidhiwa kwa idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria
Aidha, amewataka wanachi waendelee kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wanapowatilia mashaka wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.
 
 
Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA