MCHUNGAJI MTIKILA AFARIKI AJALINI.

SUNDAY, OCTOBER 4, 2015

MCH MTIKILA AFARIKI AJALINI

Na John Gagarini, Chalinze
 
MWANASIASA Mkongwe hapa nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama ChaDemocratic Party (DP) Mchungaji Christopher Mtikila (62) amefariki dunia na watu wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
 
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jafary Mohamed alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Msolwa Barabara Kuu ya Dar es Salaam Morogoro wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
 
Kamanda Mohamed alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 11:45 Alfajiri wakitokea mkoani Njombe wakiwa na gari aina ya Toyota Corola lenye namba za usajili T189 AGM lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye George Steven (31) maarufu Ponera mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam.
 
"Gari hilo likiwa na abiria watatuakiwemo marehemu mkazi wa Mikocheni B, lilikuwa kwenye mwendo wa kasi liliacha njia na kuserereka pembeni mwa barabara kasha kupinduka ambapo marehemu alirushwa nje ya gari na kupoteza maisha papo hapo,"alisema Kamanda Mohamed.
 
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na dereva wa gari hio, Mchungaji Patrick Mgaya (57) na Ally Mohamed (42) wote wakazi wa Jijini Dar es Salaam ambao wote walikimbizwa kweye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi pamoja na kuhifadhi mwili wa marehemu.
 
"Chanzo caha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa dereva huyo ambao ulisababisha ashindwe kulimudu gari hilo na kuserereka pembeni ya barabara kasha kupinduka na kupelekea kifo hico cha kusikitisha cha mwanasiasa huyo," alisema Kamanda Mohamed.
 
Hata hivyo taarifa kutoka eneo la tukio zilisemakuwa mara baada ya ajali hiyo wahanga hao hawakuweza kupata msaada kwani eneo hilo halina makazi ya watu.
 
mwisho. 
 
 

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA