ADHA YA MAJI BAGAMOYO.


ADHA YA MAJI KIJIJI CHA GONGO KATA YA MKANGE JIMBO LA CHALINZE WILAYA YA BAGAMOYO PWANI





Na John Gagarini, Mkange
WANANCHI wa Kijiji cha Gongo kata ya Mkange wilayani Bagamoyo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ambapo huweka foleni ya kuchota maji kwenye kisima kilichopo kijijini hapo baada ya wiki mbili.
Kutokana na usosefu huo wa maji wananchi hao wamekuwa wakinunua maji ya bomba ndoo ya lita 20 kati ya shilingi 1,000 na shilingi 1,500 maji ambayo huuzwa kwenye magari au pikipiki hivyo kuwafanya wajikute hawapati maendeleo kutokana na gharama kubwa kuzitumia kununulia maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa kampeni wa mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete, kwenye kata ya Mkange mwananchi wa Kijiji hicho Hungilo Nyoka alisema kuwa maji yamewafanya washindwe kupata maendeleo.
Nyoka alisema kila kaya inatakiwa ichote madumu manne ili angalau kila mmoja apate baada ya hapo maji hukatika ambapo inatakiwa mtu asubirie tena na mzunguko huo hufanya foleni ya mtu mmoja kufikiwa tena baada ya wiki mbili kwani hapa kuna wananchi 1,690.
Alisema changamoto kubwa kwao ni maji ambayo yamekuwa yakiwafanya washindwe kufanya shughuli za maendeleo ipasavyo kwani hata wakipata fedha kutokana na shughuli zao fedha zote huishia kununulia maji.
“Tunawaomba wahusika kutuangalia kwa jicho la huruma maji kwetu ni kikwazo cha kupata maendeleo kwani hata ukipata fedha kiasi gani zote zinaishia kwenye maji hivyo tunaomba tuchimbiwe kisima kwani kilichopo maji ni kidogo sana yanatoka kila baada ya saa moja yanakatika,” alisema Nyoka.
Aidha alisema kuwa maji wanayokunywa ni ya bomba lakini yanatoka vijiji jirani vya Matipwili ambako kuna umbali wa kilomita 11 na kijiji cha Mkange kilomita tisa na alisema kuwa chanzo cha maji ya kisima kutotoka ipasavyo ni kwamba waliochimba kisima hawakuchimba hadi kuuukuta mwamba ambapo chini ya mwamba ndiyo kuna maji mengi.
“Tunaomba wadau wa masula ya maendeleo kutusaidia kuweza kupata maji kwani tunashindwa hata kujiletea maendeleo kutokana ukosefu wa maji na wkati mwingine watoto hushindwa kwenda shule endapo maji yanakuwa ya shida kwani hawawezi kwenda wachafua kwani mimi kwa siku hutumia madumu matatu hadi matano kwa siku,” alisema Nyoka.
Kwa upande wake mgombea udiwani kupitia CCM Injinia Juma Mgweno alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa sana lakini atahakikisha maji yanapatikana kwa kuita wadau mbalimbali ili waweze kuwachimbia kisima.
Naye mgombea wa Ubunge kupitia CCM Ridhiwani Kikwete alisema kuwa visima viwili vilivypo kijiji hapo havitoi maji ambapo kimoja kinahitaji pampu ambayo imeharibika atahakikisha inapatikana mpya ili kuwaondolea kero wananchi wa kijiji hicho.
Ridhiwani alisema kuwa mbali ya kuhakikisha pampu mpya inapatikana pia kuna mradi mwingine wa mjai toka Matipwili na ule wa Wami Chalinze atahakikisha maji yanafika kwani mradi huo utavifikia vijiji na vitongoji ambavyo havikupata maji katika awamu mbili zilizopita vitafikiwa na awamu hii.
Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA