KONGAMANO LA MAFUTA NA GESI
Ben Komba/Pwani-Tanzania/21-03-2014/11:33
Watanzania wametakiwa kutobweteka kutokana na taarifa
za kugunduliwa gesi na mafuta maeneo mbalimbali ya nchini kwani rasilimali hiyo
haibaki milele, na kutoa msisitizo kuendelea kufanya kazi za uzalishaji mali kwa
bidii katika sekta zote ili kujenga uchumi endelevu.
Katibu kiongozi Ikulu, BALOZI OMBEN SEFUE ameyasema
hayo wakati wa ufunguzi wa kongamano la viongozi wa Mkoa wa Pwani kuhusu
Rasilimali gesi asilia, Mafuta na madini
kwa amani na maendeleo ya Tanzania lililofanyika mjini Bagamoyo mkoa wa Pwani.
BALOZI SEFUE amewakumbusha Watanzania kuwa Tanzania
bado ni nchi maskini na tukipata tamaa kuwa tupuuzie sekta nyingine kama elimu,
kilimo na harakati nyingine za kiuchumi au kila eneo ambalo linakuwa na rasilimali
za gesi na mafuta kuamua kuhodhi utajiri huo nako kunaweza kuleta magawanyiko
kama taifa.
BALOZI SEFUE amekubaliana na dhana ya rasilimali
inayopatikana eneo husika kuanza kunufaisha wakazi wa hapo lakini sio eneo
husika kuhodhi kabisa rasilimali hiyo pekee bali rasilimali yoyote
inayopatikana iwe kwa faida ya Taifa zima kwa lengo la kujenga mshikamano.
Amebainisha mpaka sasa serikali imeshauunda kamati
maalum ya wataalam ambayo itakuwa na wajibu kutafuta mbinu bora za mgawanyo wa
mapato yanayotokana na rasilimali ya mafuta na gesi.
BALOZI SEFUE amekazia kuwa Watu makini na waaminifu
wenye weledi wa kusimamia na kuendeleza rasilimali ya nchi wanahitajika ili
kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea.
Akizungumza katika kongamano hilo Mkurugenzi mtendaji
wa Shirika la Petrol Tanzania, BW.YONAH KILAGANE amesema ujazo wa gesi iliyopo
nchini ni sawa na mafuta ghafi takriban ya ujazo wa tani bilioni 1.1 au mapipa
bilioni 8.835.
BW.KILAGANE amefafanua kuwa maeneo ambayo imegunduliwa
gesi ni Mkuranga katika mkoa wa Pwani, Kiliwani,Songosongo, Mnazi Bay na Ntorya
na ili gesi hiyo iweze kutumika hakuna budi kuwepo kwa miundombinu madhubuti ya
shughuli.
Ikiwa pamoja na mitambo ya kusafishia gesi, mitambo ya
kusafirishia gesi-bomba au meli maalum na kubuni mradi mkubwa ambao utaweza
kutumia gesi hiyo kwa lengo kuimarisha uchumi wa nchi na ili kukamilika
hatua hiyo inachukua miaka takriban 9
mpaka 12.
END.
Comments
Post a Comment