WAKALA WA HALMASHAURI AKWAA KISIKI.

Ben Komba/Pwani-Tanzania/11/20/2013 10:22:20 AM

Wakala wa ukusanyaji wa ada ya maegesho mjini Kibaha ya MSOLOPA INVESTMENT COMPANY LTD, imewataka wananchi kuelewa lengo la zoezi wanaloliendesha katika suala zima la uboreshaji wa mazingira ya mji wa Kibaha.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha, BW. IBRAHIM MAULID MSOLOPA amesema wao kazi yao kubwa ni kukusanya madeni ya taasisi mbalimbali kwa makubaliano maalum.

BW.MSOLOPA ameongeza wajibu wao mjini Kibaha ni kuhakikisha wanasimamia mpango mzima wa kuupanga mji wa Kibaha ,ikiwa pamoja na kukusanya ada ya maegesho ambayo imepingwa vikali na wakazi wenye magari na wasio na magari kutokana na halmashauri kutotenga eneo la maegesho, ingawa kuna maeneo ambayo yangeweza kutumika kama maegesho ya muda.

Akitetea hatua ya Kampuni yake kukusanya ada ya maegesho, BW.MSOLOPA amebainisha yeye yupo pale kisheria ikiwa pamoja na kuingia mkataba na halmashauri wa kukusanya ada ya maegesho na takataka.

Amebainisha kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi ambao hawataki kabisa zoezi hilo kutekelezwa kutokana na kudai kuwa kukosekana na ushirikishwaji wa wananchi katika kupatiwa elimu juu ya suala hilo ambapo na wao wangepata nafasi ya kuchangia mawazo.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Kibaha, BI.JENIFA OMOLO ameelezea kusikia sintofahamu kati ya wakala wa ukusanyaji wa ada ya maegesho na wananchi, na hivyo yeye kwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la uchaguzi Kibaha mjini wataandaa kikao na kuongea na wananchi juu ya suala hilo.

Katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na harakati mbalimbali za wananchi kusigishana na halmashauri ya mji wa Kibaha kwa kile kinachodaiwa kuwepo na sheria nyingi kandamizi zenye lengo la kumnyonya mwananchi wa kawaida, ambazo kwa njia moja au nyingine zimekuwa zikisababisha vurugu za hapa na pale.

END.

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA