WITO KWA VIONGOZI WA UMMA.
Taarifa hii iliyotolewa kwa hisani ya Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani kupitia msemaji wake HASSAN JUMA imebainisha kuwa
Viongozi wa Serikali za Mitaa wameaswa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu iliyopo kwa watumishi wa umma wakati wa kutekeleza wajibu wao kwa wananchi.
hayo yamesemwa na Bw. Daniel Machunda kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani katika Warsha ya siku moja iliyohusisha makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kukuza uelewa wa wananchi kuhusu rushwa na kuhimiza uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi.
Bw. Machunda ameeleza kuwa suala la uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali za mitaa ni jambo la wajibu na wanapaswa kuhakikisha wanatenda haki katika maeneo wanayoyasimamia pamoja na kuhakikisha rushwa haina nafasi kwenye maeneo yao wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kuelewa kuwa kwa sasa wananchi wana uelewa mkubwa na wanajua haki zao, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria ili kuepusha chuki dhidi ya wananchi kwa serikali yao na kuwataka wale amabao watashindwa kutimiza wajibu wao waachie ngazi.
Nae kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Southern Africa Extension Unit (SAET) Bi. Blizabeth Ligate ameeleza kuwa hii ni mara ya pili ya mradi huo kufanya warsha inayolenga kupanua uelewa wa wananchi kuhusu rushwa, haki za msingi za raia na uwajibikaji wa watumishi wa umma chini ya ufadhili wa foundation for civil society (FCS) ambapo katika awamu ya kwanza, mradi huo uliweza kutekelezwa katika halmashauri mbili za Mkoa wa Pwani ambazo ni Bagamoyo na Kibaha zilizohusishwa kata kumi ambazo ni Maili Moja, Tumbi, Mkuza, Visiga, Picha ya Ndege, Dunda, Magomeni,Chalinze, Vigwaza, Msata pamoja na Kiwangwa ambapo awamu hiyo ilianzia kutekelezwa Agosti 2008 na kuhitimishwa Nov 2010.
Aidha Bi. Ligate amefafanua kuwa kwa sasa mradi huo umeendelea kupanuka kwa kuongezeka halmashauri ya wilaya ya mkuranga, hivyo ni matarajio ya asasi hiyo kuona wananchi wanatumia uelewa walioupata ili waweze kusimamia haki zao za msingi katika kupiga vita rushwa na kupanua uwajibikaji kwa wale wenye kutoa huduma kwa jamii.
Ameongeza kuwa asasi yao imeamua kutoa elimu kuanzia ngazi ya chini kwa kuwa bado elimu ni ndogo katika dhana nzima ya rushwa na wamejipanga kuhakikisha kuwa wanapunguza rushwa kwa kuendelea kutoa elimu katika mikoa mingine hapa nchini kwa sikum zijazo.
Warsha hiyo ya siku moja iliyoandaliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali (NGOs) ya Southern Africa Extension Unit ilifanyika katika ukumbi wa Blue Nile Hotel Kibaha na kuhusisha wadau toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii kutoka katika kata za halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bagamoyo na Kisarawe.
Comments
Post a Comment