VIONGOZI WA DINI WAKUTANA NA JESHI LA POLISI.
Ben Komba/Pwani-Tanzania/12/10/22/04:29:49 PM
Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limeelezea kushangazwa kwake na hatua ya wahuni kuchoma makanisa na kuharibu mali za serikali kwa kisingizio cha muungano.
Katika taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa viongozi wa dini katika suala zima la kutambua mchango wao katika kuleta amani na utulivu katika jamii, Kaimu Kamanda wa mkoa wa Pwani, SALEH MBAGA amesema vitendo vinavyofanyika hivi sasa hapa nchini vinatia doa amani na usalama wa nchi yetu.
BW. MBAGA amewashukuru viongozi wa dini hususan ya Kiislamu kwa kuweza kuwashika waumini wao wasifanye maandamano ya vurugu kama ilivyotokea Mkoa wa Dar es Saalam na Zanzibar, na kwa kutambua hilo Jeshi la Polisi liumeona vyema kukaa pamoja na viongozi wa dini ili kupata njia ya pamoja za amani ili kuendeleza ushirikiano wetu uliodumu kwa muda mrefu.
Amebainisha kuwa Jeshi la Polisi kwa upande wake wanaamini kuwa kuna misingi ambayo ikifuatwa vyema italiweka Taifa pazuri, kwa kuifikia jamii husika na kuijumuisha, kwa kujenga na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na jamii mbalimbali, kuweka mazingira ya uwazi, maelewano mazuri na hali ya kuaminiana baina ya jamii mbalimbali na Jeshi la Polisi.
Naye SHEIKH SALUM MKUMBA wa Msikiti wa Tumbi ambao upo mkabala na makanisa ya Kikristo amelezea kushangazwa kwake na tabia iliyozuka hivi karibuni ya baadhi ya wahuni kuanzisha vurugu kwa kisingizio cha Uislamu na hasa ikizingatiwa kwa muda mrefu kumekuwepo na mahusiano mema kati ya pande hizi mbili.
Na ameliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kufanya vikao hivi mara kwa mara badala ya kungojea majanga yatokee na ndipo wachukue hatua ya kukutana na viongozi wa dini, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuzuia kabisa vitendo hivyo kwani Jeshi hilo litaweza kupata taarifa zozote zenye lengo la kuharibu amani ya nchi kwa kisingizio cha dini.
Naye Mchungaji wa KKKT, GEORGE MWAISAKA amesema suala la imani sio kitu cha kuweza kuwafanya watu wapagawe, na hasa kutokana na mchanganyiko mkubwa wa kiimani uliopo miongoni mwa wanajamii wa Tanzania, na akijitolea mfano yeye mwenyewe kuwa pamoja na kuwa mchungaji lakini Dada yake ameolewa na Muislamu na hilo Halisumbui kabisa amani na utulivu wa familia yao.
Mchungaji MWAISAKA amelaani tabia ya serikali kufumbuia macho hali ya uvunjifu wa amani unaofanywa na vikundi vinavyojiita vya Kiislamu, na kutokana na kuwepo muingiliano katika Pwani na Dar es Saalam kuna uwezekano mkubwa wa vitendo hivyo kuambukizwa katika mkoa huu, na kukumbusha kuwa vita havina macho havichangui mtu wala dini na kutakuwa hakuna muda wa kumuabudu Mungu tena kwa utullivu uliokubalika kiimani.
END.
Comments
Post a Comment