FEDHA INAPOPINDISHA SHERIA

Ben Komba/Pwani-Tanzania/13 February 2015
Mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji EWURA imekemea utaratibu wa baadhi ya halmashauri nchini kutoa kiholela vibali vya kujenga vituo vya mafuta kinyume na matakwa ya mamlaka hiyo.

Msemaji wa mamlaka hiyo,BW.TITUS KAGUO amemueleza mwandishi wa Habari hizi kuwa kuna baadhi ya halmashauri zimekuwa zinatoa vibali vya kujenga vituo vya mafuta kiholela bila kuzingatia vigezo vinavyotolewa na EWURA.

BW.KAGUO ameongeza baada ya halmashauri hizo kuvurunda ndipo mzigo unapoiangukia EWURA, Amesema hayo kufuatia hatua ya mwandishi wa Habari hizi kuhoji juu kuendelea kujengwa kwa vituo vya mafuta katika mji wa Kibaha, Kitu ambacho kilipigwa marufuku na Aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Pwani, BIBI.AMINA MRISHO.
Ambapo amefafanua kuwa kwa mfano kituo cha mafuta kipya cha LAKE OIL kilichojengwa maeneo ya Picha ya Ndege mjini Kibaha, ambacho tayari kimeshapokea order ya kusimamisha ujenzi lakini wakapuuza amri hiyo inayoambatana na faini ya shilingi milioni 7.
Nayo kwa upande wake Halmashauri ya mji wa Kibaha imemtoza faini ya shilingi milioni 9, Mfanyabiashara anayemiliki vituo vya mafuta vya LAKE OIL kwa kukiuka taratibu za mipango miji kwa kuanza kwanza ujenzi na baadaye kuomba kibali cha ujenzi ikiwa pamoja na kujenga nje ya eneo lake.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Kibaha, BI.JENIFA OMOLO amesema kuwa mfanyabiashara huyo amekutwa na adhabu hiyo baada ya kukiuka taratibu za mipango miji ya mji wa Kibaha kwa kujiongezea eneo bila kufuata taratibu.

BI.OMOLO ameongeza kuwa kufuatia hali hiyo kamati ya madiwani ya mipango miji imezuru eneo hilo na kuchukua uamuzi wa kumpa adhabu mfanyabiashara huyo, kwa kumuamrisha kubomoa eneo ambalo ameongeza na kusimamisha ujenzi.

Na kwa sasa amepeleka maombi mapya ya kutaka kujenga kituo cha mafuta katika eneo hilo badala ya kuifanya kuwa kituo cha magari yake binafsi ambacho kingetumika k,ujazia mafuta na kwa matengenezo ya magari yake, yaani kubadilisha matumizi ya eneo, suala ambalo halmashauri ya mji wa Kibaha bado haijalitolea maamuzi.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya mipango miji ya halmashauri ya mji wa Kibaha ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kamati yao imezuru eneo hilo baada ya kuwepo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa mipango miji, na kuchukua uamuzi wa kusimamisha ujenzi uliokuwa unaendelea katika eneo hilo lililopo Picha ya Ndege mjini Kibaha.
Lakini mjumbe huyo ameongeza kuwa pamoja na kuchukuliwa hatua hizo, mfanyabiashara huyo amepuuza suala la kusimamisha ujenzi, ingawa amelipa faini ya shilingi milioni 9 kama alivyobainisha Mkurugenzi, Lakini ameendelea tene na ujenzi kuvuka eneo ambalo limesababisha kupigwa faini hali ambayo inaleta taswira tofauti miongoni mwa watu wanaofuatilia kwa karibu sakata hili.

Na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Kibaha alipoulizwa iwapo watampiga tena faini kutokana nay eye kujenga tena eneo alilokatazwa, alishindwa kutoa jibu na badala yake alizungumzia juu ya mfanyabiashara huyo kuomba halmashauri ya mji wa Kibaha kumruhusu kubadilisha matumizi ya eneo.

Kutokana na kujitokeza hali hiyo wadadisi wa mambo wamesikitishwa na baadhi ya wafanyabiashara kutumia kufahamika kwao na baadhi ya wakubwa na fedha walizonazo kupindisha taratibu za kiutendaji na hivyo kuathiri utoaji wa haki.


END.


Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA