SOGA WAJIPANGA VYEMA KULINDA MISITU.



Ben Komba/Pwani-Tanzania/12/23/2013 10:53:31 AM

Wananchi katika Kata ya Soga wilayani Kibaha wametakiwa kusaidiana na wakala wa serikali wa misitu- TFS- kwa kuziunga mkono kamati za maliasili wakati wa utekelezaji majukumu yao badala ya kuwa kikwazo.

Mtendaji wa Kata ya Soga, BW. BERT MFALAMAGOHA amesema kamati za maliasili za vijiji zimekuwa zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa na wananchi kuanza kuwanyooshea vidole wanapotekeleza wajibu wao.

BW.MFALAMAGOHA amepongeza hatua ya wakala misitu Tanzania kwa kutoa elimu kwa jamii inayozungukwa na msitu wa Ruvu kusini, ili waweze kuitunza na kuilinda misitu kwa faida ya maeneo husika.

Amefafanua kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa toka kuanzishwa kwa mradi wa mama misitu katika ukanda huo wa Ruvu  Kusini ambapo sasa wananchi wametambua wajibu wao katika kulinda na kutunza misitu ya maeneo yanayowazunguka.

Mratibu wa Mama misitu Ruvu Kusini, BW.YAHYA MTONDA  amesema kuwa anaamini wananchi wa Soga wana nafasi nzuri ya kuwa mabalozi wazuri kuhusiana na masuala ya utunzaji na ulinzi wa  misitu ya asili.

BW.MTONDA ameongeza kuwa kampeni hiyo inashirikisha makundi mbali ya kijamii ili kuwapa nafasi ya wananchi kuelewa kuwa jambo lile ni kwa faida yao kwa kufuata taratibu zilizowekwa kuhusiana na utaratibu wa matumizi wa mazao ya misitu.

Mratibu wa mama misitu, BW. MTONDA amewasisitiza wananchi kuibua miradi inayohusiana na misitu badala ya kukariri miradi ileile ambayo imezoeleka.

END.

Comments

Popular posts from this blog

MAFUNZO YA UREFA