WASIOONA KIBAHA WAJADILI KATIBA.
Ben Komba/Pwani-Tanzania/Sunday, 10 June, 2012/10:34:24
Chama cha wasioona wilaya ya Kibaha kimezungumzia suala zima la mchakato wa uandikaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa kuhakikisha haki za watu wasioona zinaboreshwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwakilishi wa wasioona Kibaha, BW. ROBERT BUNDALA amesema watu wenye ulemavu hususani wasioona wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu na kwa masuala mengi ya kijamii kutokana na sera na sheria mbalimbali kutoonyesha ni kwa namna gani tunastahili kuhudumiwa na kushirikishwa katika maamuzi ya mipango mbalimbali ya manedeleo ya Taifa.
BW. BUNDALA ameongeza kuwa kupitia fursa hii ya mabadiliko ya katiba wanaamini kwamba ni nafasi pekee wanayotakiwa kuitumia ili kujumuisha mahitaji yetu katika katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na kufanya nchi iwe na katiba jumuishi ambayo kwa kawaida huwa ndio sheria mama ya nchi.
Ameitaka serikali kujifunza kutoka nchi jirani ya Uganda na Rwanda jinsi zilivyoweka sera nzuri za kuhudumia watu wenye ulemavu amba kwa kiasi kikubwa wamepiga hatu katika kujumuisha masuala ya watu wenye ulemavu kwenye mipango mbalimbali pamoja na kuwa na majimbo yanayowakilisha watu wenye ulemavu.
BW. BUNDALA amechukua fursa hiyo kuwaasa watu wasioona kutumia nafasi hii kikamilifu katika kuhakikisha wanatoa mapendekezo yao ambayo yatatoa kipaumbele kwa kundi hilo maalum katika jamii na wasingoje kutafutwa walipo.
Chama cha wasiiona wilaya ya Kibha ni moja ya vyama vya watu wenye ulemavu ambacho kimeanzishwa mwaka 1994 kikiwa na lengo la kusogeza karibu huduma kwa wanachama wa chama cha wasioona Tanzania ambapo mpaka sasa chama hiki kina wanachama 332 na kati ya hao ME 177 na KE 155, kwa sehemu kubwa hutoa huduma kwa wasioona na jamii kwa ujumla wake.
END.
Comments
Post a Comment