RAIS KIKWETE AZINDUA UJENZI BARABARA-MSATA - BAGAMOYO.
Ben Komba/Pwani-Tanzania/09/18/2012/18:37:04
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. JAKAYA KIKWETE amewataka madereva kuwa makini wanapoendesha magari yao ili kuepusha vifo na majeruhi, ambapo katika kipindi cha mwaka 2011 watu 3100 walikufa katika ajali za barabara na kati yao wengine zaidi ya elfu 22 walijeruhiwa katika ajali hizo.
DKT. KIKWETE ameongea hayo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Msata- Makofia-Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 64, ambapo amesisitiza kwa madereva kuwa makini wanapoendesha magari ili kutopotosha nia ya serikali kueneza mtandao wa barabara zenye kiwango cha lami nchi nzima.
DKT. KIKWETE amefafanua kuwa barabara hiyo itafungua fursa ya maendeleo kwa wakazi wa Bagamoyo na vitongoji vyake hasa kwa kuzingatia kuwa itakuwa ni kichocheo cha maendeleo hususan kwa wakulima wa kilimo cha mananasi wa Kiwangwa ambao kutokana na ubovu wa barabara uliokuwepo m,ananasi yao yalikuwa yanaozea mashambani wakati wa kipindi cha mvua.
Aidha amewaasa wakazi wa maeneo hayo hayo kuwa macho na ugonjwa hatari wa ukimwi hasa kutokana na barabara hiyo kunuwiwa kutumika kwa magari yote yanayotoka kaskazini mwa Tanzania na nchi za jirani, na kutokana na hilo madwereva wa malori wanaweza kuwa chanzo kikubwa cha maambukizi hayo kutokana na desturi ya kuwa na nyumba ndogo karibu kila kituo.
Naye Waziri wa ujenzi BW. JOHN POMBE MAGUFULI amebainisha kuwa barabara hiyo inatarajiwa kugharimu shilingi zaidi ya bilioni 95, ambazo ni kwa kila kitu ambacho kinahusiana na mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni Mwakani, fedha hizo ni fedha ambazo zimetokana na mapato ya ndani.
BW. MAGUFULI ameweka wazi kwa kuwataka wananchi na watendaji wa ardhi kutokugusaa kabisa maeneo ambayo yanajuliukana kama hifadhi ya barabara na kama mtu akikaidi atavunjiwa bila kulipwa fidia yoyote, Aidha amechukua fursa hiyo kumkemea mkandarasi mshauri M. CONSULT kwa kushindwa kufanya makadirio sahihi ya mahitaji jumla ya mradi huo.
Serikali ya Tanzania imejiwekea malengo ya kujenga kilometa 11,000 za lami kukunganisha mikoa na wilaya mbalimbali hadi itakapofika mwaka 2015, ili kurahisisha uendeshaji wa shughuli za kiuchumi katika kuhakikisha kunakuwepo maendeleo ya haraka miongoni mwa watu wa kawaida kwa kuimarisha miundombinu ambayo ndio uti wa mgongo wa uchumi wowote duniani.
END.
Comments
Post a Comment