MICHAEL DADA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linapenda kuuthibitishia umma juu ya kifo cha Michael William maarufu kama Michael dada aliyeuwawa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.
Ndugu wanahabari, Michael William alikutwa na umauti mnamo tarehe 15/09/2016 majira ya saa 16:00 alasiri kufuatia kushambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha hasira kali kufuatia kudaiwa kuwateka watoto wawili.
Ndugu wanahabari, marehemu aliwateka nyara watoto wawili Furaha Justine 11 mwanafunzi wa darasa la 4 shule ya msingi Kibaha na Brigita Mashaka 6 mwanafunzi wa chekechea ya Mama Kawili ambao walikuwa wakicheza rede mtaani kwao karibu na Bar ya Lekashingo Kata ya Picha ya Ndege Wilaya ya Kibaha kwa kuwarubuni wampeleke mtaa wa Lulanzi kwenda kuchukua mizigo yake huko na alikuwa hapafahamu.
Watoto hao walimkubalia na kuanza kuongozana nae kuelekea Lulanzi lakini wakiwa njia ghafla ilitokea gari aina ya Toyota Noah ambayo haikuweza kufahamika namba yake mara moja na kuondoka na watoto hao ambao waliondoka nao na kwenda kuwatelekeza kwenye pori la Shirika la Elimu Kibaha karibu na Shule ya Sekondari Tumbi ambapo aliwapeleka kwenye pori hilo kwa lengo la kujaribu kubaka.
Ndugu wanahabari, wakati marehemu akiwa na watoto hao walipokaribia bwawa la maji machafu lililopo kwenye eneo hilo, mtoto mkubwa aliweza kukimbia na kwenda kuomba msaada ndipo kundi la watu lilipojitokeza na kuanza kumtafuta mtuhumiwa huyo, nae alipobaini juu ya kundi hilo kumfuatilia alianza kukimbia na wananchi hao walimkamata kisha kumshambulia hadi kupoteza maisha.
Uchunguzi wa awali tuliofanya Jeshi la Polisi tumeweza kubaini kuwa marehemu ni mhalifu mzoefu na alikuwa akifanya matukio ya uhalifu ya mara kwa mara ikiwemo ubakaji na wizi wa mifugo ambapo alishawahi kukamatwa na kufikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Kibaha baada ya kuiba ng’ombe wanne lakini aliachiwa huru yeye na mwenzake Said Mohammed kutokana na mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani baada ya kuwa amepata ng’ombe wake na yeye kutofika katika mahakama hiyo kutoa ushahidi hii ilikuwa ni kesi iliyofunguliwa KBA/STPU/02/2014.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani tunapenda kutoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sharia mkononi na badala yake wawafikishe wale wanaotenda makosa mbele ya vyombo vya sheria ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Pia tunatoa rai kwa jamii kujenga utamaduni wa kujitokeza kutoa ushahidi kwenye mahakama zetu pindi wanapotakiwa kufanya hivyo ili kazi kubwa inayofanywa katika upelelezi na ukamataji matunda yake yaweze kuonekana kwani kinyume cha kutokujitokeza kutoa ushahidi itahesabika ni kulea wahalifu kwenye maeneo yetu.
Imetolewa na
Boniveture Mushongi – ACP
KAMANDA WA POLISI (M) PWANI
Comments
Post a Comment